Thursday 28 July 2016

WORLD HEPATITIS DAY

HEPATITIS (HOMA YA INI)
Constantine Ntanguligwa(MD student Muhimbili university of health and allied sciences)
 2130hrs 28th July 2016

Karibu tuzungumze:

Leo tarehe 28 July ni siku ya homa ya Ini(hepatitis) duniani. Ini kama ilivyo moyo na tofauti na viungo vingine kama figo iko peke yake hivyo, kukiwa na shida kwenye ini madhara huwa moja kwa moja sababu haina usaidizi wa mwenzake. Hasara nyingine iliyopo ni kwamba kama ambavyo unaweza kuwekewa figo nyingine kutoka kwa mtu, Ini ni moja ya viungo ambapo ni kazi kufanya hivi sababu ili kupata ini lazma mtu mwingine apoteze maisha kwasababu kila mtu ana ini moja tu, si kama figo.

Leo katika kuadhimisha siku ya homa ya Ini duniani, nitakufahamisha mambo yafuatayo:
  1. HOMA YA INI NI NINI NA AINA ZAKE?
  2. HATARI YA UGONJWA HUU NA UHUSIANO NA MAGONJWA MENGINE YA INI
  3. NIFANYEJE NISIUPATE
Pengine wewe ni kama watu wengine, hujawahi kufikiria sana kuhusu Ini. Labda kwa vile hausikii kiungo hiki kama vile ambavyo unaweza kuhisi Moyo unadunda. 

Ini lina kazi kubwa sana katika mwili wako kama vile kuchuja na kujaribu kuharibu sumu yote inayoingia mwilini, kuhifadhi damu kwa mda na kusaidia kuhifadhi baadhi ya vitu muhimu vya mwili kama chakula cha wanga kama "ghala" la mwili pia kutengeneza "bile"(maji maji yanayotoka kwenye nyongo ukiipasua ndani) ambayo ni kemikali muhimu sana kukusaidia katika kula vyakula vya mafuta na kazi nyingine nyingi sana na zinazoweka kufanya maisha yao yakawa hatarini mara moja mambo yasipokwenda sawa.

Homa ya ini ni pale ambapo Ini lako linakuwa limevimba(hepatic inflammation). Imegawanyika katika aina tano. A,B,C,D na E kulingana na aina ya kirusi kinachosababisha. Hizi husambazwa kwa njia tofauti kutegemea na aina.

1.HEPATITIS A
Husambazwa kwa kugusa kinyesi cha mtu aliyekuwa na aina hii ya ugonjwa. Hivyo kuna umuhimu sana wa kuzingatia usafi wa mahala tunapoishi na kulinda mikono yetu. Kinyesi hiki pia tunaweza kukipata katika chakula au maji yasiyozingatia usafi na usalama.

2.HEPATITIS B
Aina hii inaongoza kwa kuua. Ni aina ya hatari sana. Hii husambazwa na kugusana na maji maji ya mwili(body fluids) kama damu au kutumia vitu vyenye ncha kali vinavyoweza kusababisha maji maji haya kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, pia kwa ngono au pia kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto katika kujifungua. Mbaya zaidi, kwa aina hii hata kwa jasho unaweza kupata. Hii ni hatari mno ndo maana hivi karibuni mfano, hapo Muhimbili hospitali ya taifa na chuo, wafanyakazi na wanafunzi wamepewa chanjo ili kujilinda na aina hii ya hatari.

3.HEPATITIS C
Usambazwaji wa huu ni kama wa aina B. Huu pia ni hatari sana kama aina B, unaongoza kwa kuua sana pia.

4.HEPATITIS D
Usambazwaji wa huu ni kama wa aina B

5.HEPATITIS E
Usambazwaji wa huu ni kama aina A kwa kinyesi.

Dalili zake huisiwa pale ambapo kazi ya ini inapoanza kuacha kufanya kazi na kuleta madhara yanayoonekana mfano "bile" huwa ni rangi ya njano njano hivi(ukiipasua nyongo mfano ya kuku utaona). Sasa kama ini lako litashindwa kufanya kazi "bile" itasambaa maeneo mbalimbali ya mwili na utaanza kuwa wa njano mfano machoni na kwenye ngozi labda kwasababu ya utengenezaji uliopitiliza kiasi au kuziba au kuharibika kwa mfumo husika unaosafirisha "bile" kwenda sehemu husika ambapo ni kwenye utumbo mdogo(small intestine). Unaweza kupata pia mkojo ulio "dark', kuchoka kusio kawaida, kichefuchefu na maumivu ya sehemu ya tumbo.

HATARI YA UGONJWA HUU.
Ugonjwa huu huweza kusababisha hatari ya kupoteza maisha kwani huweza kusababisha magonjwa mengine zaidi kama Kansa ya Ini(haitibiki), huweza kusababisha kuacha/kushindwa kufanya kazi ini(hepatic liver failure) na kuharibika kwa Ini kusikorekebishika(cirrhosis- Irreversible liver damage).
Magonjwa yote haya ni hatari kwa maisha yako. Hupelekea kifo ndani ya mda mfupi sana kwani Ini ni kiungo kilichopo peke yake hakina msaidizi na hivyo ini likiharibika sumu nyingi sana hujikusanya mwilini.

NIFANYEJE ILI NISIUPATE?
Kinachoua Ini ni kuingiza sumu mwilini kupita kiasi. Hivyo ini linazidiwa kazi yake na kusababisha sumu nyingi sana kujikusanya na kupelekea kuliua na kuliharibu.
Sumu hizo zinaweza kuwa Pombe, madawa mengine ya kulevya na baadhi ya madawa ya hospitalini na sababu nyingine ambazo zipo nje ya uwezo wetu kama kugusana na wagonjwa wenye magonjwa haya au kupata hivi virusi kwa njia yoyote ile kama ngono n.k.

Ni vema ukipata mda upate kupima kama unao ili upewe chanjo sababu unasambaa sana.

Tukazie zaidi kwenye vile vyanzo tunavyoweza kujizuia. Hivyo unapokula na kunywa kitu chochote angalia kiasi unachokula au kunywa hasa kama si kitu asilia yani vya kiwandani. Hasa Pombe ndo tatizo kubwa sana hapa. Jizuie kunywa pombe kupita kiasi (soma kwenye blog hii makala inayohusu Pombe na ujue kiasi kinachoshauriwa). Usifanye ngono zembe.

Mtu wangu wa nguvu. Vitu hivi vyote tunaweza kujizuia, hivyo jitahidi kufuata ushauri. Leo ni siku ya homa ya Ini duniani. Shirika la Afya duniani kuona umuhimu wa Ini na vifo vinavyoendelea kwa kasi kwa ugonjwa huu, imeamua kutenga siku hii ili ujifunze na uwe macho kuhusu homa hii hatari. Mjulishe/mshirikishe(share) na mwenzako umlinde.


AFYA YAKO, MAISHA YAKO, MIKONONI MWAKO.

Mpaka siku nyingine tena.

12 comments: