Wednesday, 24 August 2016

ADHABU NA MABADILIKO YA TABIA-AFYA

ADHABU AU MAONYO KATIKA KUBADILI TABIA YA MTU
Constantine Ntanguligwa(MD student Muhimbili university of health and allied sciences)
 1215hrs 24th August 2016

Karibu tuzungumze:

Ni wangapi tumechapwa na wazazi wetu baada ya kukosea nyumbani? Ni wangapi tumepigwa na rula vidoleni na mwalimu mwalimu wa hesabu pale ambapo tumekosea kujumlisha darasani? Ni wangapi tumewanyima chakula wafanyakazi wetu wa ndani sababu alisahau kumbadilisha mwanao nepi? Lakini pia, ni wangapi wamewachoma moto vidole watoto wao kwasababu ya udokozi?

Labda kabla sijaanza, niseme kwanini nimeamua kuongelea kuhusu adhabu leo. Afya ya binadamu, Si pale tu ambapo mtu anaumwa au kutokuumwa magonjwa mbalimbali kama malaria. Afya hujumisha maisha yote ya mwanadamu. Hali yake kimwili, kiakili(kisaikolojia), mazingira anayoishi na jamii kwa ujumla. Vyote hivi ni "afya" ya mwanadamu.

Adhabu ni kitu kinachotambulika na kukubalika katika ulimwengu wa wanasaikolojia. Adhabu hutumika kama njia ya kufanya mtu asirudie kosa endapo tu itatolewa kwa usahihi. Leo tutajua nakujibu maswali yafuatayo:

  1. ADHABU INAWEZA KUSABABISHA KOSA LISIRUDIWE AU KUTOSABABISHA MABADILIKO YOYOTE, JE ADHABU INATAKIWA KUWA VIPI?
  2. BAADA YA KUTOA ADHABU, JE KUNA KITU NATAKIWA KUFANYA ILI NIHAKIKISHE INAFANYA KAZI INAVYOTAKIWA?
Kwa mazoea, huwa tunamfanyia mtu vitendo au matukio yasiyomridhisha au yasiyompendeza au yanayokatisha tamaa mtu mara tu baada ya kufanya kosa au kuonesha tabia mbaya ambayo hupelekea mabadiliko ya tabia hiyo. Huweza kuwa faini, kufungwa, kupigwa, kufelishwa, kufukuzwa kazi/shule na kupewa barua ya onyo. Vitu hivi huitwa "aversive events" kwenye saikolojia, hili ni somo lefu linalojitegemea.

Adhabu ni kitendo yakuikandamiza tabia mbaya kwa kufanya vitendo hai(active supression). Adhabu si lazima ilete maumivu kwa mtu. Adhabu hutofautiana kuanzia zile zinazoleta madhara madogo mpaka zile zinazoweza kupelekea ulemavu wa mtu kabisa ila mwisho wa siku lengo la mtoaji likiwa kubadili mienendo mibaya kwa mlengwa.

Adhabu huweza kuwa kwa mifumo mitatu au aina tatu:
  • "Aversive events" kama nilivyoielezea hapo juu.
  • Kuondoa faida zinazodhaniwa kuwepo na muhusika au raha baada ya kufanya kosa flani au kuwa na tabia mbaya. Hasa kwa watoto.
  • Kufanya kazi ili kukandamiza tabia flani.
1.AVERSIVE EVENTS:
Hizi hugawanyika sehemu mbili. 
  • Sehemu ya kwanza ni pale ambapo utamfanyia mtu kwa vitendo atakavyohisi kwa kuona au kugusa(physical perception) mfano kwa mupata maumivu. Kama vile kumchapa fimbo au kumfinya masikio kama ni mtoto.
  • Sehemu ya pili ni pale ambapo utamfanyia vitu atakavyohisi kiakili kuwa si sahihi mfano, pale atakapotaka kufanya kosa halafu ukatikisa kichwa kumaanisha hapana. Pale atakapofanya kosa halafu ukakunja uso akajua umekasirishwa na anachofanya hivyo hutambua akilini mwake na kuacha mara moja, pale atakapofanya kosa halafu ukamnyoshea kidole au pale atakapo kuomba kwenda club na ukamwambia hapana kila mara mwisho wa siku ataona kuwa hauridhishwi nacho kisha akaacha kukuomba.
2.KUONDOA "FAIDA"/RAHA
Kama nilivyosema hapo awali kuwa, kuna watu ambao hufanya makosa au huwa na tabia mbaya inayoendelea kwasababu kuna faida anayoiona yeye anaipata baada ya kufanya hayo. Mfano mtoto asipofanya kazi za shuleni nyumbani kwasababu ya TV ukamkataza kuangalia TV kwa wiki moja. Atahisi anapitwa kama ni tamthilia na mara nyingine hatarudia hasa atakapofika shuleni na kukuta wenzake wanasimuliana kilichotokea kwenye tamthilia jana yake. Kama anapewa Ada akalipe na halipi kwa wakati na kwenda kufanya matumizi yake na hatimaye kukopa kwa wenzake na kulipa ada kwa kuchelewa labda kwa mazoea kuwa hafanywi kitu akimwelezea("kumdanganya danganya kwa maneno kidogo") mwalimu mkuu huwa anamuacha hivyo mnaweka faini kubwa isiyohitaji maelezo ambapo ataacha kwa kuona hamna maelezo tena yanayosikilizwa bali ni faini tu. Au kutoruhusiwa kuja shule mpaka utakapolipa hata kama unasababu ya msingi ya kutolipa.

3.KUFANYA KAZI
Hapa ni pale mtu anapofanya kosa au kuonesha tabia mbaya na kufanyishwa kazi kama malipizi ya tabia hiyo. Kazi hii mara nyingi huhusiana moja kwa moja na kosa lile na huweza kuwa kulazimishwa kufanya kinyume chake. mfano, mtu anapotupa takataka ovyo nje, utamwambia asafishe uwanja wote. mtoto anapomwaga chakula mezani makusudi huweza kuambiwa asafishe meza na kudeki sehemu wanayotumia kula, lakini pia mtu anapokosea kuandika jina lake utamwambia aliandike kwa usahihi mara 50.

Kunakitu tunaita "reinforcements"/viimarishi. Zenyewe hutumika kuendeleza tabia fulani. Mfano, mtoto wako anapofaulu halafu ukampa zawadi ya kitu alichokuwa anakitamani sana, hii itamjengea hamu ya kuendelea kufanya juhudi za kufaulu aendelee kupata zawadi hizo. Si lazima kutoa vitu, unaweza kuimarisha tabia kwa kunyima pia. Mfano, kama wafanyakazi wako wana sheria ya kumaliza kazi ijumaa na kwa wasiomaliza kwa wakati hutakiwa kurudi kazini wikendi lakini wanaomaliza ijumaa wanapata likizo wikendi. Kuwambia warudi wikendi ni kuwanyima uhuru ambao utapelekea kufanya kazi kwa bidii na kuimarisha tabia hii ya kumaliza kwa wakati.

TOFAUTI YA REINFORCEMENTS/VIIMARISHI NA PUNISHMENT/ADHABU: viimarishi hulenga hasa kuimarisha tabia fulani na adhabu hulenga kukandamiza tabia flani.

Hivi vinaingiliana na huweza kuchanganywa lakini ni vitu tofauti. Hii inamaanisha ni vema vitu hivi viwili vikatumika kwa pamoja. Mfano, mtoto anapokuwa na kiburi, unaweza kumchapa fimbo na matokeo yake anaweza kukuchukia na kukuona mbaya lakini kwa yale mazuri aliyonayo ukimpongeza baadaye atabadilika na kukuona kumbe si kama alivyokudhania una malengo mazuri na yeye. Hivyo inashauriwa kutumia njia zote mbili. Hivyo ni vema baada ya adhabu ukatafuta njii ya kuimarisha tabia nzuri uliyolenga kuijenga.

MADHARA YA ADHABU:
Madhara ni mengi kutokana na njia unayotumia hasa ikiwa si sahihi. mfano kuchukiwa, kukimbia shule, kutoroka nyumbani, kulia sana, kisasi na nidhamu ya woga.
Mfano, mtoto wako ni mwizi na mdokozi:
 Mtu mmoja yeye amemchoma moto vidole na mwingine amemchapa fimbo.
  •  Aliyemchoma vidole kuna hatari kubwa mwanao akakimbia nyumbani na pengine kwenda kuendeleza wizi huko anapoenda.
  •  Lakini, anayemchapa anafanya njia sahihi kwani ni uzito unaostahili kwa kesi hii na ni vema zaidi baada ya hapo ukaangalia chanzo cha kwanini mwanao ni mdokozi.                                  
Pengine wewe mzazi humuweka kwenye vishawishi vya kumuacha mwanao aende shule wenzake wakiwa wanakula wewe humpi hela ya matumizi shuleni na kuishia kuwaibia wenzake huko shuleni au hata kuiba nyumbani anapoona hela. Lakini utakapokuwa unamfungashia mfano chakula anachokipenda shuleni na kumpa hela ndogo ya matumizi kama atanunua pipi mfano utakuwa umetoa adhabu na umeimarisha(reinforce) tabia nzuri unayotaka awe nayo.

Mfano mwingine, mwanao hasomi na kagoma kwenda shule kwasababu anaamini kuwa wapo wengi wamefanikiwa na hawajasoma nakukukupa mifano kama Diamond Platnumz, Ronaldo na Messi. 

  • Mmoja akamwambia mwanae kama hutaki kusoma ondoka kwangu nisikuone ambayo ni adhabu tayari kumfukuza kwako hapa.
  • mwingine akamwambia mwanaye kuwa usinipande kichwani, kwa kuwa wewe ni mwanangu utafanya yale ninayokuongoza mimi na utakapofika umri wa kujitegemea fanya utakacho amua lakini si kwa sasa hivyo unaenda shule na nakupa kazi ya kuniandikia watu kumi waliofanikiwa bila kusoma na kumi waliofanikiwa kwa kusoma, uorodheshe historia za maisha yao na mwisho uainishe wapi waliofanikiwa kirahisi na kupita njia rahisi kufikia mafanikio yako. 

Tunakubaliana kuwa wote wanaweza kuwa sahihi kulingana na mazingira ingawa wa kwanza anaweza kumpa ushawishi mwanae kutoroka nyumbani na hata hivyo maisha yakimshinda huko atarudi amejifunza lakini huyu wa pili ametoa suluhisho lenye kiimarishi/reinforcements kwani kwa kuandika hayo aliyomwambia atajifunza kuwa shule ni chaguo zuri zaidi lenye unafuu zaidi.

HIVYO UNAPOTOA ADHABU NI VEMA UKATAFUTA NAMNA/UPENYO WA KUTOA KIIMARISHI TABIA PIA(REINFORCEMENT)

VIBOKO SHULENI:
Serikali imeagiza viboko kutotumika shuleni. Wakitoa sababu kuwa inasababisha utoro shuleni. Hii ni kweli kabisa kulingana na namna viboko hivyo vilivyokuwa vinatumika kwa baadhi ya walimu kusaka heshima ya lazima au sifa bila kuzingatia matumizi sahihi ya viboko hivyo.
Viboko vikitumika shuleni, huweza kuwa na msaada mkubwa kwa wakati sahihi, kwa kiasi sahihi na kwa nia ya dhati.

Cha muhimu, tutumie adhabu sahihi lengo likiwa kubadilisha tabia za watu na kuzuia madhara yaliyosababishwa kutokea tena. Chanzo kiangaliwe na reinforcement(viimarishi tabia) vihusike kwenye vyanzo hivyo.

Swali: Wazazi wanaotumia adhabu zilizozidi kipimo, watoto wao huwa watukutu zaidi. Je hii ni kweli?
Until next time.





2 comments:

  1. I appreciate most people especially parents don't know how punishment should be, it's a very good education.

    ReplyDelete